VITUO VYA UTAFITI WA KILIMO VYAFANYA TATHIMINI YA PROGRAMU ZA UTAFITI.
VITUO VYA UTAFITI WA KILIMO VYAFANYA TATHMINI YA PROGRAMU ZA UTAFITI
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia vituo vya Mlingano, Mikocheni na Kibaha, imehitimisha kikao cha siku mbili cha mapitio ya shughuli za utafiti zilizotekelezwa chini ya programu za ndani kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Kikao hicho kilifanyika tarehe 07 - 08/01/2026, kilifanyika katika Ukumbi wa Pope John Paul II, Chumbageni jijini Tanga, kikiwakutanisha watafiti na wadau wa kilimo wapatao 70.
Kikao hicho kilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa Mhe. Dkt.Batilda Buriani ambapo kabla ya ufunguzi alitembelea mabanda ya maonyesho na kujionea teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na TARI, ikiwemo uzalishaji wa ramani za udongo kwa ajili ya kilimo cha kidijitali, uzalishaji wa miche bora kwa teknolojia ya chupa (Tissue Culture).
uzalishaji wa miche ya matunda, viungo, na viazi vitamu pamoja na uongezaji thamani wa mazao kama nazi.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Dkt. Batilda Burian aliipongeza TARI kwa kazi kubwa inayofanya kubadilisha maisha ya wananchi kupitia tafiti zenye tija.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alisisitiza kushirikisha Vijana akiwataka watafiti kuhakikisha tafiti hizo zinawafikia na kuwasaidia vijana wengi ambao wanahitaji teknolojia rahisi ili kufanya kilimo chenye matokeo chanya.
Kutokana na umuhimu wa utafiti kwa maendeleo ya kilimo, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa mkoa umetenga ekari 1,000 katika Wilaya ya Mkinga kwa ajili ya kuongeza maeneo ya utafiti, uzalishaji wa mbegu za awali, na hifadhi ya vinasaba vya mbegu hizo.
Pia, alitoa wito kwa TARI kuanzisha mashamba ya mfano na kutoa elimu ya uzalishaji wa uyoga na mbogamboga ndani ya Jiji la Tanga ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa mjini, hasa vijana.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, aliainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, ikiwemo uchakavu wa mitambo ya uzalishaji na uhaba wa ardhi ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu bora kwa kiwango kikubwa.
Akijibu changamoto hizo, Mhe. Batilda alibainisha kuwa mchakato wa kupata eneo lingine katika Wilaya ya Pangani unaendelea vyema, mbali na zile eneo lililotengwa wilayani Mkinga kwa ajili ya shughuli za mbegu.
Kama ishara ya kuunga mkono juhudi za mkoa katika kilimo cha mazao ya kimkakati, Mkurugenzi Mkuu wa TARI alimkabidhi Mhe. Mkuu wa Mkoa miche bora ya karafuu 10,000. Miche hiyo inatarajiwa kugawiwa kwa wakulima wa Wilaya za Muheza na Mkinga ambako zao hilo hustawi vizuri.
Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba na kupokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge, Ndugu Kambona, pamoja na viongozi waandamizi kutoka Makao Makuu ya TARI Dodoma.