TARI YASHIRIKI MKUTANO WA NNE WA KIKANDA WA SAYANSI,TEKNOLOJIA NA UBUNIFU-EAC 2026.
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeshiriki katika mkutano wa nne wa kikanda wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (4th EAC Regional Science, Technology and Innovation Conference) jijini Kigali, Rwanda.
Mkutano huu ulioanza tarehe 31 Machi, 2026 hadi tarehe 1 April, 2026 unalenga kuhimiza matumizi ya Akili Unde (AI) katika kuchochea maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Thabit Kombo, alihimiza wataalam kutoka Tanzania na Afrika Mashariki kuwa wabunifu na wavumbuzi wa teknolojia zinazotatua changamoto halisi za jamii, badala ya kuwa watumiaji wa teknolojia kutoka nje ya nchi.
TARI, ikiiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Thomas Bwana ilipata fursa ya kubadilishana uzoefu na wadau wa Kikanda na Kimataifa na kujadili nafasi ya Akili Unde (AI) katika kuboresha tafiti za kilimo, kuongeza tija na kuimarisha mifumo ya uzalishaji na masoko ya mazao.
Mkutano huu pia ulihudhuriwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Dkt. Habib Kambanga pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi,mashirika na asasi za kiraia kutoka Tanzania.
Kufanyika kwa Mkutano huu ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa katika kukuza teknolojia bunifu katika mageuzi ya kilimo, sayansi na teknolojia kwa ujumla.