Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

NAIBU KATIBU MKUU KILUNDUMYA AAGIZA JENGO LA UTAWALA TARI KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI SITA.
13 Jan, 2026
NAIBU KATIBU MKUU KILUNDUMYA AAGIZA JENGO LA UTAWALA TARI KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI SITA.

NAIBU KATIBU MKUU KILUNDUMYA AAGIZA JENGO LA UTAWALA TARI KUKAMILIKA NDANI YA MIEZI SITA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (Umwagiliaji na Zana za Kilimo), Mhe. Eng. Athumani J. Kilundumya, ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuhakikisha ujenzi wa jengo jipya la utawala unakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.

Mhe. Kilundumya alitoa agizo hilo tarehe 9 Januari, 2026, wakati alipotembelea Taasisi hiyo Jijini Dodoma. Alieleza kuwa Wizara tayari imepata fedha za kutosha kwa ajili ya mradi huo, hivyo hakuna sababu itakayokubalika kuchelewesha utekelezaji wake.

"Wizara imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi huu. Niagize TARI kuhakikisha inafanya uchaguzi wa wahandisi wenye ujuzi na kuendelea na taratibu za ununuzi wa vifaa pamoja na kukamilisha ujenzi ndani ya miezi sita bila ucheleweshaji wowote, alisisitiza Eng. Kilundumya.”

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu alipata fursa ya kutembelea idara mbalimbali na amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, kwa utendaji wake. Alibainisha kuwa TARI imekuwa kioo cha Wizara ya Kilimo kupitia kazi zake za utafiti ambazo zimekuwa zikigusa na kuimarisha maisha ya Watanzania wengi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, aliishukuru Wizara ya Kilimo kwa msaada wake wa kudumu, hususani katika uboreshaji wa miundombinu. Alibainisha kuwa Wizara imetoa takribani shilingi bilioni 1.5 ambazo zimeelekezwa katika kutatua changamoto mbalimbali za watumishi wa taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Baada ya kukamilisha ziara ya Makao Makuu, Eng. Kilundumya alitembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Makutopora. Akiwa kituoni hapo, alitembelea kiwanda kidogo na kujionea shughuli za  usindikaji wa mvinyo.

Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dkt. Amachus James alitoa maelezo kuhusu hatua mbalimbali za usindikaji wa mvinyo, kuanzia maandalizi ya zabibu hadi kufikia hatua ya mwisho ya bidhaa hiyo kuingia sokoni.

Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Kilimo, Bw. James Kibamba, pamoja na wakuu wa idara na vitengo vya TARI.