DKT. THOMAS BWANA AHIMIZA UWAJIBIKAJI NA MAGEUZI YA KIBIASHARA TARI MAKUTOPORA
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Thomas Bwana, amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika Kituo cha TARI Makutupora jijini Dodoma mnamo tarehe 1-2 Oktoba, 2026, yenye lengo la kuimarisha ufanisi wa kiutendaji na kutangaza dira mpya ya taasisi hiyo.
Akizungumza na watumishi wa kituo hicho, Dkt. Bwana amewahimiza kuzingatia ushirikiano, nidhamu, na haki zinazoendana na uwajibikaji.
"Utendaji kazi lazima uzingatie kanuni za utumishi wa umma. Kila mtumishi anapaswa kutimiza wajibu wake kikamilifu kwanza, kabla ya kudai haki na stahiki zake," alisisitiza Dkt. Bwana.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu alitangaza mageuzi makubwa ya taasisi hiyo kuelekea mfumo wa kibiashara. Chini ya mwelekeo huu mpya, uzalishaji wa mbegu na mazao utafanywa kimkakati kwa kulenga soko la uhakika. Lengo kuu ni kuongeza tija na mapato, kupunguza upotevu wa rasilimali na kuifanya TARI kuwa kitovu cha kibiashara kinachochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kabla ya kuhitimisha ziara hiyo,Dkt. Bwana alifanya ziara ya kukagua miradi na mashamba ya utafiti ambako alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya utafiti na kilimo inayotekelezwa kituoni hapo, ikiwemo:
Shamba la majaribio ya rozela, utafiti wa mbolea za kibaiolojia, matumizi ya bakteria, kuongeza uzalishaji wa choroko katika maeneo ya nyanda kame pamoja na vipando vya zao la zabibu, shamba la majaribio la tufaaa, pamoja na bustani ya matunda ya ndizi na maembe yenye lengo la kuimarisha uzalishaji endelevu na usalama wa chakula nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Makutupora, Dkt. Paul Saidia, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa ziara hiyo na kubainisha kuwa imekuwa chachu kubwa ya mabadiliko. Alimuahidi Dkt. Bwana kuwa uongozi na watumishi wa kituo hicho wamejipanga kuleta mabadiliko ya haraka ili kufikia maono na malengo yaliyowekwa.
Katika ziara hiyo ya kikazi, Dkt. Bwana aliambatana na viongozi mbalimbali wa makao makuu, akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Bi. Grace Sylivester; Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu, Dkt. George Sonda; na Kaimu Mkurugenzi wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano, Bi. Evelyne Mpasha.