WAZIRI WA KILIMO AZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA KUMI YA TARI
Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Daniel Chongolo (Mb) amezindua rasmi maadhimisho ya miaka kumi ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na kuagiza sherehe za maadhimisho hayo zifanyike Agosti, 2026 katika kipindi cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane ili kutoa fursa kwa wadau wengi zaidi kushiriki.
Mhe. Chongolo ametoa agizo hilo Aprili 23, 2026 katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo (kilimo iv) na kueleza ushiriki wake katika maadhimisho hayo huku akipongeza mchango mkubwa wa TARI katika kuleta mageuzi ya sekta ya utafiti wa mbegu nchini ndani ya kipindi cha miaka kumi.
Aidha, Mheshimiwa Chongolo alifananisha mchango huo wa TARI na uimara wa nyumba ambao hutegemea msingi na kubainisha kuwa TARI ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Katika hafla ya uzinduzi huo, Mhe. Chongolo alizindua jezi maalum ya TARI itakayotumika katika TARI Marathon ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya TARI.Pia alikabidhi jumla ya pikipiki 71 kwa taasisi hiyo. Vitendea kazi hivyo vinatarajiwa kuongeza ufanisi kwa watafiti wa TARI katika vituo vya utafiti na mashamba ya majaribio kote nchini, hivyo kuharakisha utoaji wa matokeo ya tafiti kwa wakulima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Thomas Bwana amemshukuru Mhe. Chongolo kwa kukubali kujumuika na TARI katika hafla ya uzinduzi wa miaka kumi ya taasisi hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa David Silinde (Mb), Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo,Mheshimiwa Athumani Kilundumya,Menejimenti ya TARI na watumishi kutoka vituo vya TARI Hombolo na TARI Makutopola.