MWIGULU AIPONGEZA TARI KWA TAFITI ZENYE TIJA KATIKA SEKTA YA KILIMO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Lameck Mwigulu Nchemba (Mb), ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kufanya tafiti zenye tija ambazo zimeendelea kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Pongezi hizo amezitoa mnamo Agosti 1, 2026, alipotembelea banda la TARI wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nane Nane 2026), yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya Dkt. John Samuel Malecela, jijini Dodoma.
Akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na mawaziri kutoka wizara mbalimbali, Dkt. Nchemba alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba alipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na taasisi hiyo katika kufanya tafiti za kilimo na kuendeleza teknolojia mbalimbali bunifu zinazolenga kuongeza tija na kuinua uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na uzalishaji wa mbegu bora za zabibu na tufaa, pamoja na ubunifu wa teknolojia ya zana ya kupandia mbegu inayojulikana kama Rafiki Planter, ambayo inalenga kuongeza ufanisi na tija kwa wakulima.
Dkt. Nchemba alieleza kuwa jitihada za TARI katika kuendeleza tafiti na teknolojia bunifu zina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa wakulima pamoja na taifa kwa ujumla