Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

WAZIRI MKUU AKABIDHI NDEGE NYUKI KWA TARI KUIMARISHA UTAFITI NA MATUMIZI ENDELEVU YA ZANA ZA KILIMO.
05 Feb, 2026
WAZIRI MKUU AKABIDHI NDEGE NYUKI KWA TARI KUIMARISHA UTAFITI NA MATUMIZI ENDELEVU YA ZANA ZA KILIMO.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mwigulu Nchemba (MB) ameikabidhi Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ndege nyuki (Drone) ili kuongeza ufanisi katika tafiti mbali mbali za kilimo.

Mhe. Nchemba amekabidhi ndege nyuki (drone) hiyo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Afrika kuhusu Matumizi endelevu ya zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization - ACSAM) uliofanyika   Jijini Dar es Salaam. Hii ni mara ya kwanza kwa Mkutano huo ambao umeratibiwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) kufanyika nchini Tanzania.

Awali, katika taarifa yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na  Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi za Nigeria, Somalia, Niger, Afrika ya Kati, Rwanda na Senegal, Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo alibainisha kuwa Mkutano huu pamoja na mambo mengine utajadili masuala mbalimbali kuhusu zana za kilimo pamoja na kupata uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu namna bora ya kuimarisha matumizi ya zana za kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa zinazozingatia mabadiliko ya tabia nchi.

 Mhe. Chongolo ameongeza kuwa mkutano huu pia umewakutanisha pamoja Watunga Sera, Wawakilishi wa Serikali wakiwemo Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi mbambali za Afrika, Wadau wa Maendeleo, Watafiti, Wakulima, Asasi za Kiraia na Mashirika ya Sekta binafsi yanayojihusisha na maendeleo ya vijijini na uendelezaji wa Sekta ya Kilimo ili kupeana uelewa wa namna bora ya kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye Sekta ya Kilimo.

Mbali na ufunguzi wa Mkutano huo, Mhe. Nchemba pia amezindua rasmi Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo wa Awamu ya Pili (2026 hadi 2035) ambao umelenga kuimarisha matumizi, utengenezaji na uendelezaji wa zana za kilimo.