Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

TARI, FAO WAJADILI MKAKATI WA KUKUZA KILIMO CHA TENDE.
23 Jul, 2026
TARI, FAO WAJADILI MKAKATI WA KUKUZA KILIMO CHA TENDE.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imepokea ugeni kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) nchini, lenye lengo la kuimarisha na kuendeleza kilimo cha tende kama mkakati wa kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ziara hiyo imefanyika Julai 21, 2026, katika ukumbi wa Maabara ya Kilimo Mtumba, jijini Dodoma. Wajumbe wa FAO walipata fursa ya kujionea mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo unaoratibiwa na TARI Kituo cha Hombolo, ukifadhiliwa na FAO na kusimamiwa na Wizara ya Kilimo.

Mradi huu wa tende kwa sasa unatekelezwa katika maeneo ya wilaya ya Chamwino ikihusisha kijiji cha Chalinze Nyama pamoja na vijiji vya Mvumi Mission, Makangwa, na Handali sanjari na eneo la Hombolo jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, alieleza kuwa mradi huo unalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo ya nyanda kame, kwa kuwa zao la tende lina uwezo mkubwa wa kuhimili ukame.

Dkt. Bwana aliongeza kuwa kupitia mradi huo, mbegu mpya za kisasa zimesambazwa kwa wakulima ili kuondoa kilimo cha mazoea na kuongeza tija katika uzalishaji.

"Kutokana na mwitikio mkubwa wa wakulima, TARI imeanza mchakato wa kuzalisha mbegu za tende hapa nchini. Hii itasaidia kukidhi mahitaji yanayokua kwa kasi badala ya kuendelea kutegemea kuagiza mbegu kutoka nje ya nchi," alisema Dkt. Bwana.

Kwa upande wake, Mwakilishi na Mkurugenzi Mkazi wa FAO nchini Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tipo, alieleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa wakulima wana hamasa kubwa ya kulima zao hilo jipya. Alisisitiza kuwa FAO itaendelea kuunga mkono jitihada kama hizo zinazosaidia kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Mratibu wa Mradi kutoka TARI, Dkt. Nicholaus Kuboja, alibainisha kuwa hadi sasa mradi umegawa miche 55 ya tende, ambapo kila mkulima anayeshiriki amepata miche 22. Aidha, zimeanzishwa mashamba darasa matatu (3) ili kuwajengea uwezo wakulima na kurahisisha upatikanaji wa mbegu bora.

Baada ya mazungumzo hayo ujumbe huo ulitembelea Kituo cha TARI Hombolo kujionea kwa vitendo shughuli mbalimbali za uzalishaji wa mbegu za tende.