Rais Samia azidua Maabara Kuu ya Kilimo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo Agosti 08, 2025 amezindua Jengo la Maabara Kuu ya taifa ya Kilimo iliyopo Mtumba jijini Dodoma inayolenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.
Maabara hiyo inayosimamiwa na Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inauwezo wa kufanya uchunguzi wa changamoto mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija.
Miongoni mwa huduma zitakazotolewa katika jengo hilo lenye maabara 15 za kisasa ni Kuanzia uchunguzi wa afya ya udongo, utambuzi wa visumbufu vya mimea, utambuzi wa ubora wa Mbegu na maabara ya utambuzi wa viini lishe kwenye mazao.
Aidha, Maabara hiyo ya kisasa inayotarajiwa kuwa na sifa za maabara ya rufaa ya kilimo itashughulika na kupima vimelea vya sumukuvu na sumukuvu yenyewe katika mazao.
Akizindua jengo hilo, Dkt, Samia, aliagiza kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya TARI ambazo zitakuwa ni nje ya jengo hilo la Maabara.