Kamati ya Bunge Yaridhishwa na Mafanikio ya Miradi ya Umwagiliaji TARI.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji nchini.
Pongezi hizo zimetolewa kufuatia ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyofanyika tarehe 18 Machi 2026, ambapo ilitembelea na kukagua miradi ya kimkakati ya umwagiliaji katika Kituo cha TARI Hombolo.
Katika ziara hiyo, wajumbe walianza kwa kutembelea Bwawa la Hombolo, mojawapo ya mabwawa sita yanayofanyiwa ukarabati chini ya mpango wa TRIP II, unaolenga kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kuvuna maji kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, aliishukuru kamati kwa kutembelea taasisi hiyo na kutoa maelezo kuhusu mradi huo. Alieleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji unalenga kuwezesha utafiti kufanyika mwaka mzima, hata kipindi cha kiangazi bila kutegemea mvua. Hali hiyo itapunguza muda wa kukamilisha tafiti za mbegu na kuongeza uzalishaji wa mbegu bora zinazostahimili ukame, ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Aidha, kamati ilipata fursa ya kutembelea mradi wa kilimo cha tende, zao lenye thamani kubwa kiuchumi, unaolenga kuwapatia wakulima mbadala wa biashara pale mazao ya chakula yanaposhindwa kutokana na ukame, pamoja na kuongeza kipato cha kaya.
“Nia yetu ni kubuni teknolojia zinazotoa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto za wananchi, huku tukizingatia mnyororo mzima wa thamani kuanzia afya ya udongo hadi masoko, tukielekea kufikia Dira ya 2050,” alisema Dkt. Bwana.
Kwa upande wao, wajumbe wa kamati walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali, kuongeza ubia na sekta binafsi katika usambazaji wa mbegu bora, pamoja na kudhibiti kwa ukali mbegu feki sokoni ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Ziara hiyo ilihitimishwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, ambaye alieleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa miradi hiyo. Alibainisha kuwa TARI inaonyesha mwelekeo chanya wa mageuzi katika sekta ya kilimo nchini, na kuahidi kuwa kamati itaendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa lengo la kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa viwanda.