Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

KAMISHNA WA MAGEREZA ATOA RAI KWA TARI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA JESHI LA MAGEREZA TANZANIA.
14 Jul, 2026
KAMISHNA WA MAGEREZA ATOA RAI KWA TARI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA JESHI LA MAGEREZA TANZANIA.

Kamishna wa Huduma za Urekebu wa Jeshi la Magereza, CP Amina Kavirondo, ametembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, na kujionea teknolojia na ubunifu wa taasisi hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Kamishna Kavirondo ameipongeza TARI kwa mchango wake mkubwa katika kufanya tafiti zenye tija zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Aidha, ametoa wito kwa TARI kushirikiana na Jeshi la Magereza Tanzania katika kuwapatia wafungwa mafunzo ya uongezaji thamani wa mazao mbalimbali yanayofanyiwa utafiti na taasisi hiyo. Amesisitiza umuhimu wa kuwajumuisha wafungwa miongoni mwa makundi maalumu yanayonufaika na programu za mafunzo na uwezeshaji, kama ilivyo kwa makundi mengine.

Kamishna Kavirondo amesema ushirikiano huo utawajengea wafungwa ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri na kujipatia kipato halali baada ya kumaliza vifungo vyao, jambo litakalosaidia kupunguza uwezekano wa kurejea katika vitendo vya uhalifu.

"Tukiwapa maarifa na stadi za kuongeza thamani ya mazao, tunawapa fursa ya kuanza maisha mapya yenye tija na kuwa sehemu ya maendeleo ya taifa," amesisitiza.

Kwa upande wake, TARI imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuendeleza tafiti na ubunifu unaochochea maendeleo ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, pamoja na kuongeza thamani ya mazao yanayofanyiwa utafiti kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa.