TARI NA WADAU WASHIRIKIANA KUFANIKISHA MKUTANO WA MWAKA WA MRADI WA KILIMO SHADIDI(SRI)
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa Ushirikiano na Taasisi ya NIBIO wameendesha kwa ufanisi mkutano wa tatu wa mwaka kupokea matokeo ya Mradi wa Mifumo ya Kuimarisha Uzalishaji wa Mpunga Tanzania kwa kufanya kikao cha mwisho pamoja na warsha ya wadau leo tarehe 13 Machi 2026 katika Ukumbi wa St. Gaspar, jijini Dodoma. Kikao hicho kililenga kutathmini mafanikio ya utekelezaji wa mradi, kujadili mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka mikakati ya kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo cha mpunga kwa wakulima nchini.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, aliwashukuru wadau wote walioshiriki katika utekelezaji wa mradi huo pamoja na Serikali ya Norway kwa ufadhili na ushirikiano wao. Alisisitiza kuwa zao la mpunga lina nafasi muhimu katika kukuza ajira kupitia mnyororo wake wa thamani na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa. Aidha, alibainisha kuwa matumizi ya teknolojia sahihi za kilimo ni muhimu katika kuongeza tija kwa wakulima, huku akieleza kuwa tafiti zinazofanywa na TARI zina lengo la kuleta mageuzi chanya katika sekta ya kilimo na kuchangia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Dkt.Udaya Sekhar kutoka taasisi ya NIBIO akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Mradi wa SRI–Tanzania, alieleza kuwa mradi huo ulilenga kuboresha maisha ya wakulima wadogo wa mpunga kwa kuongeza uzalishaji huku ukipunguza athari kwa mazingira. Alifafanua kuwa kupitia mradi huo wakulima walipatiwa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa mpunga, matumizi ya kanuni za mbinu husishi za kuthibiti wadudu waharibifu, huduma za afya ya mmea pamoja na kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa rasilimali maji kwa ajili ya kilimo cha mpunga. Aliongeza kuwa licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika utekelezaji wake, mradi umefanikiwa kuwajengea uwezo wakulima na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya kilimo.
Akiwasilisha mada kuhusu mafaniko yaliyopatikana katika utekelezaji wa mradi huo, Mtafiti Kiongozi wa Mradi wa Kilimo Shadidi, Dkt. Atugonza Bilaro, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na ubia katika kueneza na kupanua matumizi ya teknolojia za mifumo ya kuimarisha uzalishaji wa zao la mpunga. Pia, alieleza kuwa matumizi ya Nyenzo za kilimo pamoja na ubunifu wa zana za kilimo vinavyotengenezwa ndani ya nchi zina mchango mkubwa katika kuongeza tija, huku zikitoa fursa za ajira kwa vijana na wanawake. Aidha, alibainisha kuwa mbinu ya umwagiliaji wa mpunga ambapo shamba halikai na maji muda wote. Badala yake, mkulima huacha maji yakauke kidogo kisha kumwagilia tena, huwezakusaidia kudhibiti mkusanyiko wa chumvi kwenye mashamba ya umwagiliaji. Pia hufungua fursa kwa wakulima kunufaika na masoko ya mfumo wa kusaidia kupunguza mabadiliko ya tabianchi unaotokana na hatua mbalimbali za kupunguza hewa ya ukaa.
Kwa upande wa wakulima walionufaika na mradi huo, Bi. Anna Maganga alieleza kuwa kupitia mafunzo na ushirikiano uliotolewa na TARI ameweza kuongeza tija kwenye mazao,kuanzisha vikundi vya vijana vinavyojihusisha na kilimo cha mpunga pamoja na kuanzisha darasa ili kutoa mafunzo kwa vijana ili kuwajengea ujuzi na kuwapatia fursa za kitalu Mkeka kujiajiri. Alitoa shukrani kwa TARI kwa msaada na mafunzo yaliyowawezesha kufikia mafanikio hayo.
Akifunga kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Mkurugenzi wa Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano, Dkt. Sophia Kashenge, aliipongeza timu ya mradi pamoja na wadau wote kwa juhudi zao katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uzalishaji wa chakula kupitia matumizi ya teknolojia bora za kilimo na kuhimiza wadau kuendeleza ushirikiano katika kukuza kilimo cha kisasa chenye tija na kinachovutia kwa kizazi cha sasa na kijacho. Pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji ili kuhakikisha teknolojia hizi zinaendelea kuwafikia na kuwanufaisha wakulima wengi zaidi nchini.