Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

TARI YAELIMISHA WAKULIMA JINSI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI
07 May, 2026
TARI YAELIMISHA WAKULIMA JINSI YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia kituo cha Hombolo kinachojihusisha na mazao ya nyanda kame pamoja na teknolojia zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi, imeandaa maadhimisho ya Siku ya Wakulima yaliyofanyika Mei 5, 2026 katika Kata ya Hombolo, jijini Dodoma

Maonesho hayo yamefadhiliwa na mradi wa KAFACI (Korea-Africa Food and Agriculture Cooperation Initiative), unaolenga kuendeleza teknolojia himilivu kwa mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.

Akifungua rasmi maadhimisho hayo, Meneja wa Kituo cha TARI Hombolo, Dkt. Emmanuel Chilagane, alisema lengo la tukio hilo ni kuwakutanisha wakulima, kujadili na kutatua changamoto zinazowakabili, pamoja na kuendeleza kilimo kupitia ubunifu wa teknolojia zinazokidhi mahitaji ya sekta hiyo.

Dkt. Chilagane aliongeza kuwa kituo hicho kimepanua wigo wa mazao yanayofanyiwa utafiti, ikiwa ni pamoja na ufuta, mbaazi, tende, mahindi na miche mbalimbali ya matunda. Alitoa wito kwa wakulima kushirikiana na TARI ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuinua kipato chao.

Katika maadhimisho hayo, wakulima walipata mafunzo kutoka kwa watafiti wa kituo hicho kuhusu mabadiliko ya tabianchi, athari zake katika kilimo, teknolojia za kukabiliana nayo, pamoja na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli za kilimo. Pia walipata fursa ya kutembelea mashamba ya majaribio ya uzalishaji wa mbegu bora na miche ya miti ya matunda. Takribani wakulima 250 walishiriki katika tukio hilo.

Kwa upande wake, mtaalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Bw. Stephen Zawadi aliwahimiza wakulima hao kutumia taarifa hizo ili kuchagua mazao sahihi na kuepuka kilimo cha mazoea kinachoweza kusababisha hasara.

Naye mkulima na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Hombolo Bwawani ambaye ni mnufaika, Bw. Noah Madeje, aliishukuru TARI kwa kutoa elimu kuhusu mbegu bora, matumizi sahihi ya udongo na umuhimu wa taarifa za hali ya hewa, akisema maarifa hayo yataongeza tija na kipato kwa wakulima na kuahidi kuyatumia kwa manufaa yao.

Akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia na Mahusiano wa TARI, mtafiti kutoka makao makuu ya taasisi hiyo, Bi. Stela Hangambage, alipongeza Kituo cha TARI Hombolo kwa kufanikisha tukio hilo la kila mwaka na kuwataka wakulima kuendeleza ushirikiano na taasisi hiyo ili kupata taarifa sahihi zitakazowasaidia kuboresha kilimo chao.

slot gacor