Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

TARI,WADAU WAJADILI USHIRIKIANO WA KUKUZA KILIMO CHA MUHOGO.
18 May, 2026
TARI,WADAU WAJADILI USHIRIKIANO WA KUKUZA KILIMO CHA MUHOGO.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imepokea ugeni kutoka Chuo Kikuu cha Cornell cha nchini Marekani pamoja na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya kilimo cha muhogo nchini.

Ziara hiyo imefanyika Mei 14, 2026, katika Makao Makuu ya TARI jijini Dodoma, ambapo wageni hao walipata fursa ya kujionea mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa Muhogo Bora unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya TARI, Chuo Kikuu cha Cornell na IITA.

Mradi wa Muhogo Bora, unaofadhiliwa na Chuo Kikuu cha Cornell na kuratibiwa na IITA kwa kushirikiana na TARI, unatekelezwa katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi, Singida na Rukwa. Mradi huo unalenga kuhamasisha matumizi ya mbegu bora za muhogo zinazostahimili magonjwa ya virusi, kuendeleza mbinu bora za uzalishaji pamoja na kuongeza kipato cha wakulima wadogo. Aidha, mradi huo unachangia kuimarisha usalama wa chakula na kupunguza uhaba wa mbegu bora za muhogo nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, alisema taasisi hiyo itaendelea kuwekeza katika tafiti za kisasa na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi, ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa urahisi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa IITA ambaye pia ni Mtaalamu Mshauri wa Mifumo ya Mbegu, Dkt. Kiddo Julius Mtunda, akiambatana na Prof. Hale Ann Tufan kutoka Chuo Kikuu cha Cornell pamoja na Prof. Chiedozie Egesi kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Mazao ya Mizizi ya Umudike nchini Nigeria, alisema mradi huo umefanikiwa kugawa mbegu mama vipande milioni 1.9 za muhogo kwa kushirikiana na TARI.

Alieleza kuwa kupitia mradi huo, wakulima takribani 3,996 wamefikiwa huku lishe kwa wanafunzi wa shule za msingi zaidi ya 12 katika maeneo yanayotekelezwa mradi huo ikiendelea kuimarishwa.

Baada ya kikao hicho, ujumbe huo ulitembelea Kituo cha TARI Makutopora na kujionea shughuli mbalimbali za utafiti wa zao la zabibu pamoja na shughuli za uongezaji thamani kupitia kiwanda kidogo cha usindikaji kilichopo kituoni hapo.

Kaimu Mkurugenzi wa TARI Makutopora, Mtafiti Isack Teya, aliwapatia wageni hao maelezo kuhusu aina mbalimbali za zabibu zinazolimwa katika kituo hicho, matumizi yake pamoja na mchakato wa uzalishaji wa mvinyo bora unaofanyika kituoni hapo.

slot gacor