PROF. MSOFFE AITAKA TARI KUONGEZA JUHUDI ZAIDI JUU YA UTAFITI WA ZANA ZA KILIMO.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula Prof. Peter Msoffe ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuongeza juhudi katika utafiti na ubunifu wa zana za kilimo zilizo rafiki na rahisi kutumiwa na mkulima.
Prof. Msoffe ametoa agizo hilo alipotembelea banda la TARI katika Viwanja vya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba). Pia, alipongeza jitihada zinazofanywa na TARI katika utafiti wa udongo, mbegu, visumbufu vya mimea pamoja na uongezaji thamani wa mazao mbalimbali baada ya mavuno na kueleza kuwa TARI imejijengea sifa kubwa katika uzalishaji wa mbegu bora kwa mfano mpunga aina ya SARO 5 (TXD 306) ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji na tija kwa mkulima.
Akiwa katika banda la TARI, Prof. Msoffe alibainisha kuwa, kwa sasa TARI inajulikana zaidi kwa matokeo ya utafiti wa mbegu bora na afya ya udongo lakini kwa upande wa zana za kilimo bado jitihada zaidi zinatakiwa ziongezwe katika kasi ya ubunifu wa zana bora za kilimo, rahisi na rafiki kwa mkulima ili kumpunguzia mzigo mlengwa katika shughuli za kilimo ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea kilimo endelevu, chenye tija na kinachochangia maendeleo ya sekta ya kilimo na Taifa kwa ujumla.
Wadau na wananchi mbalimbali wameendelea kutembelea banda la TARI na kupata elimu ya teknolojia za Kilimo katika mnyororo wa thamani ikiwa ni Pamoja na teknolojia baada ya mavuno. Pia, wamepata fursa ya kununua miche ya mazao mbalimbali ya migomba, matunda, mboga, viungo na vikolezo.