TARI NA WADAU WA MBEGU WAUNGANA KUTATUA KITENDAWILI CHA MASOKO.
Sekta ya mbegu nchini imeingia katika hatua mpya kufuatia ushirikiano wa karibu kati ya Wadau wa Maendeleo, Serikali na Sekta Binafsi wenye lengo la kuhakikisha mkulima hapati tu mbegu, bali anapata mbegu bora na inayokidhi mahitaji ya soko.
Katika mkutano wa siku mbili uliomalizika hivi karibuni kati ya tarehe 12 na 13 katika Ukumbi wa Mount Meru, Jijini Arusha chini ya mradi wa Accelerated Variety Turnover, wadau hao walikubaliana kuondoa pengo lililokuwepo kati ya watafiti na wafanyabiashara wa mazao ili kuharakisha mapinduzi ya kilimo nchini.
Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dkt. Thomas Bwana, alisema sekta ya kilimo ni muhimili muhimu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikitarajiwa kuchangia hadi asilimia 40 ya Pato la Taifa. Alisisitiza kuwa malengo hayo hayawezi kufikiwa iwapo wakulima wataendelea kutumia mbegu za zamani zisizoendana na mahitaji ya soko.
Alibainisha kuwa TARI imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, ambapo mwaka 2025 pekee taasisi hiyo imezalisha tani 125 za mbegu daraja la msingi ili kupunguza upungufu wa upatikanaji wa mbegu nchini.
Kwa upande wake, Dkt. Chris Ojiewo kutoka Kituo cha kimataifa cha Kuboresha Mahindi na Ngano (CIMMYT) alisema mradi wa ACCELERATE umeundwa kutatua changamoto ya kukosekana kwa uwiano kati ya uzalishaji na soko. Alieleza kuwa hapo awali wafanyabiashara walilalamikia ukosefu wa mbegu bora, huku wazalishaji wakidai kukosa soko la uhakika. Kupitia mfumo mpya, mfanyabiashara amewekwa katikati ya mnyororo wa thamani akiainisha aina ya zao analohitaji, mkulima huzalisha kwa uhakika, na mtafiti hutoa mbegu inayokidhi mahitaji hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), Nyasebwa E. Chimagu, alisema taasisi hiyo imeanza kuhamia katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha huduma. Alieleza kuwa usajili wa mbegu sasa utafanyika kwa njia ya mtandao ili kupunguza urasimu, huku kalenda za kidijitali zikianza kutumika kufuatilia mashamba ya mbegu kote nchini. Aidha, aliongeza kuwa marekebisho ya Sheria ya Mbegu yanaendelea ili kuendana na mabadiliko ya soko.
Kwa upande wa wadau wa maendeleo, Bwana Jean Claude Rubyogo wa Taasisi ya Kimataifa ya Pan-Africa Bean Research Alliance (PABRA) pamoja na Jeffrey Ehlers Gates Foundation walisisitiza kuwa mafanikio ya tafiti za kilimo hayapimwi kwa idadi ya aina mpya za mbegu zilizogunduliwa, bali kwa namna zinavyobadilisha maisha ya wakulima. Walihimiza Serikali kuendelea kuimarisha mfumo wa mbegu za daraja la Kuazimiwa Ubora (QDS) ili kuwafikia wakulima wengi zaidi, hasa wa maeneo ya vijijini.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Mkutano huu ulifungwa na Mkurugenzi wa Uhaulishaji Teknolojia Teknolojia na Mahusiano Dkt.Sophia kashenge.Aliwashukuru wadau wote walioshiriki mkutano huo na kusema TARI Inawakaribisha wadau wote kwa lengo la kuimarisha ushirikiano zaidi.