Wakulima wa Pamba Wahimizwa kuachana na Kilimo cha Mazoea ili Kuongeza Tija.
WAKULIMA WA PAMBA WAHIMIZWA KUACHANA NA KILIMO CHA MAZOEA ILI KUONGEZA TIJA.
Wakulima wa pamba nchini wamehimizwa kutumia teknolojia za kisasa za uzalishaji ikiwepo upandaji wa zao hilo kwa nafasi mpya za upandaji (sm60 x sm30) iliyogunduliwa na TARI ambazo zimekuwa chachu ya kuongezeka kwa uzalishaji wa pamba nchini.
Wito huo umetolewa Novemba 17,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt Thomas Bwana katika Mkutano wa wadau wa Mradi wa Cotton Victoria uliofanyika katika kituo cha TARI Ukiriguru (Mwanza) kwa lengo la kutathimini utekelezaji wa mradi. Amesema kutokana na matumizi ya teknolojia zilizoasisiwa na mradi huo, wakulima wameshuhudia mabadiliko makubwa katika uzalishaji.
“Kuna maeneo wakulima walikuwa wanapata chini ya kilo 500 (kwa ekari) lakini sasa hivi kuna wakulima wanapata zaidi ya kilo 1000, kwahiyo unaweza kuona kwamba ongezeko la mavuno ni kubwa kwa wale wanaotumia mbinu ambazo tumewaelekeza” Amesema Dkt Bwana na kubainisha mbinu hizo ni pamoja na kupanda kwa wakati kwa kutumia umbali wa sm60 x sm30, matumizi sahihi ya viuatilifu, na kudhibiti magugu kwa wakati.
Mradi wa Cotton Voctoria ulianza kutekelezwa mwaka 2016 ukiwa na lengo la kuinua uzalishaji wa pamba katika nchi za Tanzania, Kenya na Burudi. Hadi sasa hapa nchini, mapokeo ya teknolojia za mradi huu yamefikia asilimia 63 ya wakulima wa pamba katika Mikoa 11 inayozalisha zao hilo la kibiashara.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania Bw. Marco Mtunga amesema kuwepo kwa mradi huu kumejibu hoja ya kuongeza tija katika uzalishaji wa pamba “Maeneo kama Simiyu sehemu kubwa ya wakulima walikuwa wana sia mbegu, lakini sasa wanapanda kwa vipimo ambavyo vinatoa idadi kubwa ya miche, na hiyo ndiyo huchangia uzalishaji kuwa mkubwa kwenye eneo.” Amesema Bw. Mtunga.
Mkutano wa kutathimini utekelezaji wa mradi wa Cotton Victoria umewakutanisha wadau mbalimbali katika tasnia ya pamba wakiwemo watafiti kutoka TARI kituo cha Ukiriguru, Bodi ya Pamba, wawakilishi kutoka Wakala wa Ushirikiano wa Brazili (ABC)
na ubalozi wa Brazil nchini Tanzania, baadhi ya Maafisa kilimo na wakulima viongozi kutoka Mkoani Geita, pamoja na uwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo.