Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

TARI YASHIRIKI AFRICA AGRI EXPO 2026, YASISITIZA MATUMIZI YA UTAFITI KWA BIASHARA NA MAENDELEO
24 Sep, 2026
TARI YASHIRIKI AFRICA AGRI EXPO 2026, YASISITIZA MATUMIZI YA UTAFITI KWA BIASHARA NA MAENDELEO

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeshiriki Maonesho ya 10 ya Kilimo Afrika (Africa Agri Expo 2026), yanayofanyika tarehe 2–3 Septemba 2026 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, TARI inaendelea kuwawezesha wakulima, wafanyabiashara, wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kufahamu teknolojia, ubunifu na matokeo ya tafiti zinazolenga kuongeza tija, uzalishaji na thamani katika sekta ya kilimo.

Katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, ameshiriki katika shughuli mbalimbali na kukutana na wadau wa sekta ya kilimo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha matokeo ya utafiti yanafika kwa wananchi na kutumika katika shughuli za uzalishaji na biashara.

Akizungumza katika maonesho hayo, Dkt. Bwana amesema TARI inaendelea kuhamisha mkazo kutoka kwenye utafiti wa jadi kwenda kwenye utafiti wa kisasa unaolenga matokeo na athari chanya kwa jamii.

“Tunatoka kwenye utafiti wa jadi kwenda kwenye utafiti wa kisasa, ambapo tunahitaji kuhakikisha utafiti wetu una matokeo na athari zinazoonekana. Hatutaki utafiti ubaki kuwa utafiti pekee; tunataka teknolojia zetu zitumike kufanya biashara, kuzalisha fursa za kiuchumi na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi,” amesema.

Ameeleza kuwa TARI ina teknolojia takribani 312 zinazolenga kutoa suluhisho katika sekta ya kilimo, huku akisisitiza umuhimu wa kuangalia ni kwa kiwango gani teknolojia hizo zinatumika na kuchangia katika uzalishaji na uchumi wa wananchi.

“Tunazalisha mbegu bora, tuna rasilimali za vinasaba na Genebank kwa ajili ya kuhifadhi mbegu na vinasaba vya mimea, tunaendelea na tafiti za kuongeza thamani ya mazao, tunatoa ushauri wa kisera na tuna maabara za kisasa. Hivyo, tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha matokeo ya utafiti yanageuka kuwa fursa za biashara na maendeleo,” amesema.

Dkt. Bwana amesisitiza kuwa TARI inalenga kujenga mnyororo unaounganisha utafiti na matumizi yake katika jamii, kutoka kwenye utafiti hadi biashara, kutoka kwenye utafiti hadi mabadiliko chanya na hatimaye kutoka kwenye utafiti hadi kuboresha maisha ya wananchi.

“Lengo letu ni kutoka kwenye utafiti kwenda kwenye biashara, kutoka kwenye utafiti kwenda kwenye mabadiliko na hatimaye kutoka kwenye utafiti kwenda kwenye maisha bora kwa wananchi,” amesisitiza.

Ushiriki wa TARI katika Africa Agri Expo 2026 ni sehemu ya juhudi za Taasisi za kuendeleza ushirikiano na wadau wa sekta ya kilimo, kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kilimo na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika katika kuongeza tija, ajira, kipato na maendeleo ya wananchi.

slot gacor