Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara Ya Kilimo

TAASISI YA UTAFITI WA KILIMO TANZANIA

TARI YASHIRIKI MKUTANO WA WADAU WA KOROSHO DUNIANI.
04 Feb, 2026
TARI YASHIRIKI MKUTANO WA WADAU WA KOROSHO DUNIANI.

TARI YASHIRIKI MKUTANO WA WADAU WA KOROSHO DUNIANI

Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Thomas Bwana pamoja na Timu ya  watafiti kutoka TARI Naliendele   wako nchini Dubai kuhudhuria mkutano wa Dunia wa Wadau wa Korosho (World Cashew Conference) ikiwa ni fursa ya kushiriki majadiliano, kujifunza na kufahamu  muelekeo wa zao la korosho Duniani.

Mkutano huo wa siku tatu (tarehe 30 Januari – 1 Februari)  pamoja na mambo mengine umejadili mambo mbalimbali kuhusu muelekeo wa zao la korosho, changamoto pamoja na  fursa zilizopo katika  maendeleo ya teknolojia mbalimbali katika tasnia ya zao la korosho.

Mkutano huo ambao umekutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali Duniani  katika mnyororo wa thamani utasaidia TARI kuwa na mwelekeo sahihi wa kazi za utafiti wa zao la korosho ili kukidhi malengo ya soko la Dunia.

Vilevile katika Mkutano huu TARI imefanikiwa kufanya majadiliano na baadhi ya Taasisi na washirika wa maendelea kama GIZ, ACA na CHINA chamber of Commerce na kupenyeza mapendekezo na mawazo ya kitafiti ili kupata uwezeshaji katika maeneo mbalimbali ya kitafiti

 Washirika wa Maendeleo GIZ watafadhili  miradi 2 kwenye zao la korosho. Aidha, TARI inaangalia uwezekano zaidi wa kupata ufadhili wa GIZ kwenye masuala ya CARBON CREDIT kwenye korosho na mazao mengine

Katika hatua nyingine, TARI imepanga kushirikiana na  Taasisi ya African Cashew Alliance katika kuandaa program ya mafunzo ili  kuwajengea uwezo watafiti katika tasnia ya korosho.

Timu ya TARI iliyoambatana na Mkurugenzi Mkuu wa TARI katika Mkutano huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Naliendele Dkt. Geradina Mzena, Mtafiti kiongozi wa zao la korosho Dkt. Wilson Nene na  Mratibu wa Uhaulishaji Teknolojia Bw. Bakari Kidunda.

TARI kupitia Kituo chake cha TARI Naliendele wana jukumu mahsusi Kitaifa la kufanya utafiti  wa zao la korosho katika mnyororo wa thamani.